Pages

Thursday, December 20, 2012

ICC yapokea malalamiko ya LHRC polisi kuua raia


Written by   20/12/2012 
Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimejibiwa rasmi barua kiliyoandika katika Mahakama ya Kimataiafa ya Uhalifu (ICC), iliyopo The Hague nchini Uholanzi ambayo inalenga kulifikisha Jeshi la Polisi nchini kwenye mahakama hiyo kutokana na kuendelea kuwaua raia wasiokuwa na hatia.
Mkurugenzi wa LHRC, Dk. Hellen Kijo-Bisimba, amesema barua waliyojibiwa hivi karibuni na ICC, ni miongoni mwa maombi mengi waliyowasilisha katika vyombo vingine vya kimataifa kuviomba vichunguze uhalifu unaofanywa na Jeshi la Polisi hapa nchini dhidi ya raia.
Dk. Bisimba aliyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana.
Hata hivyo, Dk. Bisimba alisema licha ya Polisi kuendelea kuwaua raia, kituo chake kinalaani mauaji yaliyofanywa na raia dhidi ya Polisi wawili wiki iliyopita mkoani Kagera.
Wiki iliyopita, Polisi wawili waliuawa na raia wenye hasira baada ya Polisi hao kumuua raia kwa risasi wilaya ya Ngara mkoani Kagera.
Hadi sasa, watu 40 wanashikiliwa na polisi kuhusiana na mauaji hayo.
Akizungumzia uhalifu unaofanywa na Polisi hapa nchini, Dk. Bisimba alisema wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu, lakini mwaka huu matukio ya mauaji yanayofanywa na chombo hicho yamezidi kuongezeka.
“Tumejibiwa rasmi barua tuliyoandika kwa Mwendesha Mashitaka wa ICC na ameahidi kuifanyia kazi ikiwemo kufanya uchunguzi ili kubaini ukweli kwa lengo la kuchukua hatua nyingine,” alisema Dk. Bisimba.
Alifafanua kuwa kinachochangia kuwapo mauaji kwa mwaka huu, ni ukosefu wa utawala wa sheria ulionyooka hapa nchini, hatua ambayo raia na Polisi kila mmoja anamuona mwenzake kama adui.
Kwa upande wa raia kuwaua Polisi ama kuua raia mwenzao, Dk. Bisimba alisema suala hilo linaweza kushughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi na vyombo vya usalama.

Akizungumzia matukio ya mauaji kwa ujumla, Dk. Bisimba alisema mwaka huu umekuwa haueleweki kwa kuwa hali ya usalama haikuwa nzuri na watu wengi wamepoteza maisha wakiwamo raia na Polisi kwa upande mwingine.
Kuhusu kulaani mauaji ya Polisi, aliitaka jamii kubadilika na kuheshimu utawala wa sheria na kuachana na vitendo hivyo.
Alisema kama watumishi hao wakianza kuvamiwa na kuuawa na raia, ni jambo la hatari kwa nchi.
“Tunalaani kwa nguvu zote mauaji ya Polisi yaliyofanywa na raia, na ombi letu kwa jamii ni kuitaka iachane na vitendo hivi na kuzingatia utawala wa sheria,” alisema.
Alitaja baadhi ya matukio ya kuuawa Polisi ni pamoja yale yaliyotokea mkoani Mwanza, baada ya watu wasiojulikana kumpiga risasi aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Liberatus Barlow.
Wengine waliouawa na raia ni pamoja na askari Abdulrahman wa visiwani Zanzibar na hivi karibuni askari wawili mkoani Kagera.
Alisema vitendo hivyo vya mauaji kwa pande zote za raia na Polisi ni doa kwa dhana ya Polisi Jamii iliyoasisiwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema.

No comments:

Post a Comment