Mkurugenzi wa LHRC, Dk. Hellen Kijo-Bisimba, amesema barua waliyojibiwa hivi karibuni na ICC, ni miongoni mwa maombi mengi waliyowasilisha katika vyombo vingine vya kimataifa kuviomba vichunguze uhalifu unaofanywa na Jeshi la Polisi hapa nchini dhidi ya raia.
Dk. Bisimba aliyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana.
Hata hivyo, Dk. Bisimba alisema licha ya Polisi kuendelea kuwaua raia, kituo chake kinalaani mauaji yaliyofanywa na raia dhidi ya Polisi wawili wiki iliyopita mkoani Kagera.
Wiki iliyopita, Polisi wawili waliuawa na raia wenye hasira baada ya Polisi hao kumuua raia kwa risasi wilaya ya Ngara mkoani Kagera.
Hadi sasa, watu 40 wanashikiliwa na polisi kuhusiana na mauaji hayo.
Akizungumzia uhalifu unaofanywa na Polisi hapa nchini, Dk. Bisimba alisema wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu, lakini mwaka huu matukio ya mauaji yanayofanywa na chombo hicho yamezidi kuongezeka.
“Tumejibiwa rasmi barua tuliyoandika kwa Mwendesha Mashitaka wa ICC na ameahidi kuifanyia kazi ikiwemo kufanya uchunguzi ili kubaini ukweli kwa lengo la kuchukua hatua nyingine,” alisema Dk. Bisimba.
Alifafanua kuwa kinachochangia kuwapo mauaji kwa mwaka huu, ni ukosefu wa utawala wa sheria ulionyooka hapa nchini, hatua ambayo raia na Polisi kila mmoja anamuona mwenzake kama adui.
Kwa upande wa raia kuwaua Polisi ama kuua raia mwenzao, Dk. Bisimba alisema suala hilo linaweza kushughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi na vyombo vya usalama.